Matangazo
HUYU NDIYE DK. PHILEMON SENGATI MKUU MPYA WA MKOA WA SHINYANGA...ZAINAB TELACK AHAMISHIWA LINDI
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati
Na Damian Masyenene - Shinyanga
Leo Mei 15, 2021 mkoa wa Shinyanga umempata mkuu wa mkoa mpya, Dk. Philemon Sengati baada ya kudumu kwa miaka mitano na Zainab Telack aliyeuongoza mkoa huo tangu mwaka 2016 akipandishwa cheo kutoka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema.
Dk. Sengati ameteuliwa leo na Rais Samia Suluhu katika mabadiliko ya safu ya viongozi wakuu wa mikoa.
Dk. Sengati kabla ya uteuzi wa leo alikuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora, ambapo alirithi mikoba ya Aggrey Mwanri Julai 3, 2020 alipoteuliwa na Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk. John Magufuli kuchukua mikoba ya Mwanri ambaye alistaafu.
Kabla ya uteuzi huo wa kuwa RC wa mkoa wa Tabora Julai 3, mwaka jana, Dk. Sengati alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.
Kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Magu, Dk. Sengati alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dodoma akiwa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma.
Leo ameteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Shinyanga kuchukua mikoba ya Zainab Telack ambaye amehamishiwa mkoa wa Lindi, ikiwa ni miezi miezi 10 tu baada ya kuwa RC mkoani Tabora.