Wananchi wafurika banda la Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula NFRA
Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Nchini NFRA imewataka wananchi kujifunza njia bora za uhifadhi wa chakula ili kiweze kudumu kwa muda mrefu na ubora unaohitajika.
Hayo yamesemwa na NFRA wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya 45 ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo, Afisa Uhusiano wa NFRA, Angela Shangali amesema ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
Amesema, lengo la NFRA ni kuhakikisha upatikanaji wa akiba ya chakula cha kimkakati wakati wa upungufu wa chakula kwa kununua, kuhifadhi na kuzungusha na kuuza chakula kwa ufanisi na manufaa ya jamii.
Shangali amesema, taasisi yao wamekuwa wananunua chakula cha akiba kutoka katika maeneo yaliyo na ziada ya uzalishaji na kuyahifadhi katika maghala 34 yaliyopo kwa sasa.
“Tunanunua chakula kutoka kwa wakulima, na mazao hayo yanakuwa na viwango vya ubora vinavyokubalika na matumizi bora ya viuatilifu na utaratibu bora wa uhifadhi ili kuhakikisha nafaka tunazozihifadhi zinaendelea kuwa katika ubora unaohitajika”,amesema Shangali.
Aidha, amesema wanatoa elimu kwa wananchi namna bora ya uhifadhi wa chakula na huduma za kitaalamu kama unyunyuziaji na ufukizaji wa nafaka zilizohifadhiwa.
Shangali amesema, NFRA wamekuwa wanatoa pia huduma ya kukodisha maghala kwa wafanyabiashara na wakulima sambamba na upimaji wa uzito wa magari.
Akielezea kuhusu majukumu ya wakala, Shangali amesema wamekuwa na taratibu ya ununuzi wa akiba ya chakula , utoaji wa chakula kwa waathirika, uuzaji wa chakula ndani na nje ya nchi na kuongeza pato la ya Taifa na uhamishaji wa akiba ya chakula kutoka maeneo yaliyo na uzalishaji mkubwa na kuyapeleka maeneo yenye upungufu.
Amongezea na kusema, kwa sasa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula wanauza nafaka ambazo ni mtama, mpunga na mahindi.
Kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo wanaohitaji kupata huduma ya ununuzi wa nafaka wafike katika ofisi zao za kanda nchini au Makao Makuu ya NFRA Jijini Dodoma. Pia wanaweza kuwasiliana kwa njia ya barua pepe info@nfra.go.tz na wavuti www.nfra.go.tz
Afisa wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Amina Mtenda akitoa maelezo kwa wananachi waliotembelea banda lao wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya 45 ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa Jijini Dar es salaam.
Meneja Uwekezaji na Milki wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Nchini (NFRA) Eng Imani Nzobonaliba akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda lao ndani ya Maonesho ya Kimataifa ya 45 ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Wananchi wakiwa katika banda la la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Nchini (NFRA).
content://com.android.chrome.FileProvider/images/screenshot/1620891111823-1928548343.png