Matangazo
Jeshi la polisi Mkoa wa Simiyu Lakamata vifaa vya mradi wa umeme wa Rea vyenye thamani ya tsh27,984,244 vilivyokuwa vimeibiwa.
Samirah Yusuph.
Bariadi. Jeshi la polisi Mkoa wa Simiyu limekamata vifaa vya ujenzi wa mradi wa umeme wa Rea vyenye thamani ya tsh27, 984,244 vilikuwa vimepotea, vifaa hivyo vilivyolenga kukamilisha miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Katika taarifa iliyotolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu Richard Abwao imeeleza kuwa vifaa hivyo vimekamatwa katika operesheni ya usalama VII iliyoanza Julai 29, hadi Agosti 08,2021 ambapo jumla ya watuhumiwa 99 wamekamatwa kutokana na makosa mbalimbali.
Amevitaja vifaa vilivyokamatwa kuwa ni Base Plate type A & B jumla 35, Stay Wire Rollar 08 Mita 1,016, Pig Tail Bolt 300 na Barbed wire Rollar 12 Mita 2,160 vifaa vyote jumla vina thamani ya TShs 27,984,244.
"Kesi 33 zimefunguliwa katika vituo vya Polisi mbalimbali na jumla ya watuhumiwa 49 watafikishwa mahakamani ili kusomewa mashtaka, Wahumiwa 11 bado wapo chini ya uangalizi wa Polisi,"amesema Kamanda Abwao.
Aidha amesema katika operesheni hiyo pia wamekamata madawa ya kulevya aina ya Bangi kilo 4 na Mirungi kilo 270 pamoja na magari mawili yenye namba za usajili T.970 DDG aina ya RAUM na T.637 DSQ aina ya TOYOTA PROBOX yaliyopatikana na Nyara za Serikali ambazo ni nyama mbichi ya Pundamilia, nyama kavu ya Nyemela, pamoja na ngozi ya Simba,
Katika taarifa hiyo ameeleza pia wamekamata mitambo mitano ya kutengeneza pombe haramu aina ya gongo wizi wa Mifugo pamoja na wakimbizi 39 waliokuwa wanatoroka kambi ya wakimbizi Nyarugusu, Kigoma kuelekea nchi jirani ya Kenya.
Akielezea operesheni ya usalama barabarani amesema kuwa hadi sasa jumla ya makosa 476 ya usalama barabarani yamekamatwa na kukusanya faini ya tsh10,460,000.